Amesema
mtume Muhammad (Rah’ma na amani) kuwa hatoinua mja mguu wake siku ya Qiyama
mpaka aulizwe juu ya mambo manne. Moja ya mambo hayo ni kuhusiana na ujana
ambapo mja ataulizwa “Ujana wake aliutumia vipi.”
Wengi
wetu tumefanya ujana ni umri wa mtu kujiachia na kufanya majambo ambayo hayana
msingi kwenye maisha yetu ya Duniani na hata Akhera pia. Ni lazima tukubali
kuwa dunia imebadilika. Dunia ya sasa sio ile ya zamani ya kuuchezea ujana kwa
kuamini kuwa uzeeni utafanya mambo uliyoyakusudia.
Yafuatayo
ni mambo 15 ya kufanya kabla ya kupita umri wa ujana wako ambao mara nyingi ni
miaka kati ya 30 hadi 35.
1. Maliza Masomo Yako.
Ni
vizuri mtu akamaliza masomo yake kabla ya kupita umri wa ujana wake. Wameeleza
wana sayansi kuwa umri chini ya miaka 30 ni umri ambao mtu akili yake inakuwa
ni yenye nguvu na uwezo wake wa kujifunza mambo unakuwa ni wa haraka.
Hivyo ni
vizuri kijana kuutumia umri huu kumaliza masomo yake na kuhakikisha anapata
taaluma (Profession) atakayoitumia maishani mwake hasa sehemu za kazi maana
hata kazi nazo siku hizi mbali na kuangalia taaluma pia unaangaliwa umri.
2. Jifunze Fani Mbalimbali.
Mbali na
taaluma uliyoipata shuleni ni vizuri ukajifunza fani walau mbili tatu kutoka
kwenye mafunzo ya ufundi stadi. Unaweza kujifunza udereva, ufundi ujenzi,
ufundi seremala, ufundi cherehani n.k. Fani hizi zitakusaidia sana maishani
mwako aidha kwa shughuli zako binafsi au hata kwa shughuli za kukuingizia
kipato.
3. Jifunze stadi za maisha.
Kuna
mengi ya kujifunza maishani mwetu. Mfumo wetu wa elimu umeweka mbali sana
mafunzo ya stadi za maisha. Kutokana na umuhimu wake mkubwa maishani mwetu, ni
lazima kujifunza majambo haya. Vitu kama kupika, kufua, na kazi zingine za
nyumbani ni vizuri mtu akajifunza katika ujana wake. Vilevile kujifunza kuhusu
mahusiano, maisha katika jamii n.k ni mambo yanayoshauriwa sana mtu ajifunze
katika ujana wake.
4. Jifunzi Dini yako.
Mfumo wa
maisha ya mwanaadamu wenye kuelekeza zuri na baya, la kufanya na la kutofanya,
upo ndani ya dini.
Maisha
kiujumla wake yamejaa mengi. Maisha yamejumuisha mambo mazuri na pia yamejumuisha
mambo mabaya. Ni vizuri mtu akautumia umri wake wa ujana vilevile kujifunza
dini yake. Ajue kusoma kitabu cha Mola wake na vilevile ajue mambo yote ya
msingi yanayohusiana na dini yake.
5. Ijue Historia ya Familia na Ukoo wako.
Hakuna
kitu kizuri maishani kama kuijua familia yako na ukoo wako kwa ujumla wake. Jua
wapi wazazi wako walipotokea. Jua baba na mama zako wadogo kwa majina na mahala
wanapoishi. Wajue wajomba, mashangazi, makaka, madada na wote wanaoihusu
familia yako.
Hii
itatengeneza mahusiano mazuri kati yako na familia yako kiujumla na kupanga
mikakati mizuri ya kusaidiana inapotokea shida. Pia itakusaidia kujua nani
anaweza kushirikiana nawe katika harakati za kimaendeleo.
6. Anza kuweka akiba.
Chukua
mfano wa kijana mwenye umri wa miaka 15. Akisema kila siku aweke Tshs 1,000/=,
maana yake kwa mwezi anauwezo wa kuwa na Tshs 30,000/= ambapo kwa mwaka anakuwa
na Tshs 360,000/=. Kama tukisema twende hadi miaka 30, kijana huyu atajikuta
ana Tshs 5,400,000/=.
Hicho ni
kiasi kikubwa sana ambapo mtu anaweza kusema anunue kiwanja, aanze biashara, au
awekeze popote atakapo. Ila yote hiyo itatokana na kuweka akiba.
Ni
vizuri mtu akawa na utaratibu wa kuweka akiba kwenye ujana wake walau
unapofikia umri wa uzeeni basi unakuwa na kiasi cha kukusaidia kuendesha maisha
yako.
7. Anza kufanya kazi na anzisha kazi zako Binafsi.
Naam!
Kazi ndio msingi mkubwa katika kuendesha maisha yetu ya kila siku. Iwe kazi ya
kuajiriwa au kujiajiri, basi hakikisha unakuwa na kazi kabla ya kupita kwa umri
huo.
Kazi
yoyote ya halali ikifanywa vizuri, na kwa Ari basi inaweza kuleta tija kubwa
katika maisha ya mtu.
Jitahidi
kupata kazi ya halali itakayokuingizia kipato cha halali kabla ya kupitwa na
ujana wako kwani wapo wazee wengi wanahadhirika maishani mwao kwa kushindwa
kupata cha kujishughulisha nacho ujanani mwao.
8. Kuwa na utaratibu wa kujisomea.
Alisema
msomi mmoja kuwa, ukitaka kumfichia kitu mu Afrika, basi muwekee kwenye ktabu.
Hii ina maana kuwa wa Afrika wengi, watanzania tukiwemo, hatuna utaratibu wa
kujisomea.
Kwenye
kujisomea kuna faida nyingi. Mbali na kufanya akili kuwa safi muda wote pia mtu
anapata wasaa wa kujifunza vitu vipya ambavyo vinaweza kumsaidia maishani mwake
kwa sasa na baadae pia.
Ni
vizuri ukajiwekea utaratibu wa kujisomea vitabu, makala, magazeti n.k kuhusiana
na masuala ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara na mambo mengine yanayohusu maisha.
9. Jiunge na vikundi vya kijamii.
Kuna
msaada mkubwa sana mtu kuwa kwenye vikundi vinavyofanya kazi za kuhudumia
jamii. Vipo vikundi vya kifedha, michezo na utamaduni, afya, dini na vingine
vingi. Ndani ya vikundi hivi unaweza kukutana na watu wapya mnaoweza kusaidiana
katika maisha pia unaweza kutumia kama njia moja wapo ya kusaidia jamii
inayokuzunguka.
10.
Acha!
Acha! Acha! – Kuvuta Sigara, Ulevi, Uzinifu.
Asilimia
kubwa ya vijana hupenda kuvuta sigara, ulevi na hata uzinifu. Kwa sasa huenda
usiyaone madhara yake kwani ni vitu ambavyo huwa vinakula taratibu taratibu.
Ila kwa miaka ya mbeleni unaweza kuja kukutana na madhara makubwa ambayo
yanaweza kukufanya upoteze furaha ya maisha yako.
Jitahidi
sana katika ujana wako kuojihusisha na uvutaji wa sigara, ulevi na uzinifu pia
kwani gharama zake mbeleni ni kubwa mno.
11.
Funga ndoa.
Naam!
Jitahidi sana kufunga ndoa kabla ya kupitwa na ujana wako. Mbali na kupata
utulivu wa nafsi, ila itasaidia kuongeza uwajibikaji na umakini kwenye mambo
mbalimbali ya maisha yako. Pia itasaidia kupata watoto mapema ambao wanaweza
kuja kukusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yako ya mbeleni hasa katika
shughuli zako za kila siku na Biashara zako kwa ujumla.
Kubwa ni
kuheshimika katika jamii kwani asilimia kubwa ya watu waliopo kwenye ndoa huwa
wanapewa heshima kubwa kwenye jamii zao na kushirikishwa kwenye baadhi ya
majambo ya msingi.
12.
Kuwa na
Ratiba.
Ni
kawaida sana katika zama zetu kumkuta kijana hana jambo la kufanya. Yaani
ukimkurupua kumwambia akusindikize sehemu, basi atakwenda muda huo huo na
ukimuuliza huna la kufanya atakujibu ndio.
Ni
vizuri kijana akapanga muda wake na kupanga mambo yake ya siku nzima. Jifunze kuweka
ratiba ya kufanya mambo yako ya siku, wiki, mwezi na hata mwaka pia. Hii
itakusaidia kufikia malengo yako ki urahisi na kutopata muda wa kufanya vitu
visivyo na msaada maishani mwako.
13.
Tengeneza
Mtandao wa watu watakaokusaidia. baadae
Kwa
lugha ya kiingereza wanasema “Networking.” Jitahidi kuwa na network nzuri,
yenye watu wazuri na wenye manufaa maishani mwako. Hakikisha kila mtu mzuri
unayekutana nae unatengeneza nae mahusiano mazuri yatakayokunufaisha wewe na
kumnufaisha yeye pia.
Hakikisha
unapata marafiki kwenye kila idara ya kiuchumi, siasa, utamaduni na masuala ya
kijamii pia.
14.
Mazoezi!
Mazoezi! Mazoezi.
Hili ni
jambo la msingi sana kwa kijana. Hakikisha unakuwa ni mwenye kufanya mazoezi
walau mara mbili kwa wiki. Chagua mazoezi yatakayoendana na muda wako wa kazi
na muda wako wa mambo mengine. Ni vizuri kufanya mazoezi asubuhi au/na jioni.
Hii itasaidia kuuweka mwili wako vizuri na wenye afya muda wote. Vilevile
itasaidia kukuweka mbali na magonjwa madogo madogo yanayoweza kupunguza ufanisi
kwenye shuguli zako.
15.
Jifunze
Lugha za Kigeni.
Dunia ya
leo ni dunia ya utandawazi. Watu kutoka mataifa mbalimbali wanawekeza kwenye
nchi za wengine. Ni vizuri ukajifunza lugha za kigeni hasa za mataifa
yanayokuja kuwekeza kwenye nchi yako. Lugha itatanua wigo wako wa ajira,
biashara, na hata kujua tamaduni za watu wengine.
16.
Jiweke
mbali na madeni.
Hakuna
kitu kinachorudisha nyuma watu kama vile madeni. Madeni humfanya mtu kila
kipato anachopata kina kwenda kulipa madeni na badala ya kufanya maendeleo ya
maisha yake. Hivyo jitahidi sana kuepuka madeni ndani ya umri huu. Kama kuna
watu au taasisi inakudai basi fanya juu chini kulipa madeni hayo haraka na
epuka kwa hali na mali kukopa (hasa mikopo yenye riba).