Monday 25 July 2016

VITU VINNE VITAKAVYOFANYA BIASHARA YAKO ITHAMINIWE


Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusiana na wateja kudharau biashara zao au hata kutopata wateja wanaothamini biashara zao. Hii inatokana na sababu kadhaa ambazo huenda zikawa upande wa mfanyabishara au hata mteja mwenye pia.

Kuna mambo kadhaa ambayomfanya biashara anatakiwa kuyafanya ili kuifanya biashara yake kuwa na thamani kwa wateja au hata watu wengine.

1.  Jina la Biashara.
Jina la Biashara yako ndio kitu cha kwanza kitakachowafanya wateja na watu wengine waithamini Biashara hiyo. Jina ni lazima liwe jepesi, fupi na lenye kuleta maana nzuri kwa wateja uliowakusudia na jamii kwa ujumla wake. Ni lazima uwe na jina la biashara litakaloendana na Biashara yako au kile unachokifanya kwenye shughuli zako za kila siku au hata jina litakaloakisi sekta unayofanyia kazi.

Uchaguzi mbovu wa jina unaweza kufanya watu wakaidharau biashara yako na wasiwe ni wenye kuitilia umakini. Vilevile kufanya Biashara ambayo haina jina kunaweza kusababisha ukose baadhi wa wateja ambao watahisi haupo serious na biashara yako.

2.  Machapisho.
Machapisho yana umuhimu mkubwa sana kwenye kumfanya mtu aithamini biashara yako. Mbali na kutumika kwenye kutangaza Biashara, pia machapicho yanaweza kutengeneza picha nzuri kwa mteja na kumfanya ahisi kuwa upo makini na unachokifanya.

Machapisho hayo yamejumuisha Vipeperushi, Business Cards, Mabango, Kalenda, Majarida, Vitabu, Fulana, n.k. Vilevile unaweza kuchapisha nembo ya biashara yako sehemu zingine kama vile kwenye kalamu, vikombe, au hata funguo.

Hii itafanya watu waithamini biashara yako katika thamani ya hali ya juu.

3.  Tovuti.
Tovuti hufahamika kwa urahisi kama “Website”. Katika dunia ya leo mtu anaposikia au kuona biashara yako na akavutiwa nayo, basi atakachofanya ni kuingia kwenye mtandao na kutafuta tovuti yako ili ajue unachokifanya kwa undani.

Hivyo asipoona tovuti yako kwenye mtandao hatoweza kufahamu unachokifanya na hii ndio itakuwa hatua ya kwanza ya mtu kutoithamini biashara yako.

Vilevile watu wengi inapowajia dhana ya kutaka kitu cha kununua huwa wanaanza kukitafuta kitu hicho kwenye mitandao. Hivyo utakapokosa tovuti nzuri yenye utalaamu wa kutosha, basi hakuna mtu atakayeweza kukufahamu na unaweza kukosa wateja wengi sana kwenye biashara yako.

Ni vizuri kwa mfanyabiashara kuwa na tovuti nzuri, yenye gharama nafuu, itakayoelezea biashara yake kwa ujumla na hata kuweka baadhi ya ripoti na mafanikio yanayohusiana na biashara yake hiyo.

4.  Barua pepe.
Huenda kikaonekana ni kitu kidogo sana, ila barua pepe (email) ni kitu cha muhimu sana kwenye biashara za kileo.

Wafanya biashara wengi katika zama zetu hupenda kutumia simu kwa kuwasiliana na wateja wao. Ila ni lazima tutambue kuwa watu wengi hupenda kuulizia biashara kupitia barua pepe na kueleza wanayoyahitaji pia. Hii hutengeneza mahusiano yako na mteja ambapo mkishajuana vizuri ndio hufuata mazungumzo ya njia ya simu.

Hivyo ni lazima kwa mjasiriamali wa kileo kuwa na barua pepe atakayotumia kuwasiliana na wateja wake.

Hakikisha unakuwa na barua pepe iliyokaa kiofisi zaidi. Usipende kutumia barua pepe zenye @gmail.com, @yahoo.com, @hotmail.com. Barua pepe za namna hii huwa hazileti mashiko na kwa wateja makini huenda ndio ikawa hatua ya kwanza ya kutothamini biashara yako. Tumia barua pepe zenye jina lako la biashara hasa ile itakayoendana na tovuti yako. Mfano marwa@tigo.com


No comments:

Post a Comment