
Asilimia kubwa ya vijana wamekuwa kwenye moto wa kutaka kuanzisha Biashara zao wenyewe. Ila wengi wao hawajui (na wala hawazingatii) mambo muhimu ambayo mtu inabidi ayafanye kabla ya kuanzisha biashara.
Kuna maswali muhimu 20 ambayo
Mjasiriamali aliyekuwa na Malengo ya Kufika mbali anapaswa kujiuliza kabla
hajaanza kufanya Biashara yake.
Maswali hayo ni haya yafuatayo
1.
Kwa nini nataka kufanya Biashara?
Hili ndio swali la kwanza
kujiuliza. Ni lazima ujue sababu kuu zinazokufanya utake kuanzisha Biashara.
Usije ukaanzisha Biashara kwa sababu tu umemuona fulani kaanzisha basi nawe
ukaanzisha. Wengi wamepoteza muelekeo wa Biashara zao kutokana na sababu kuwa
walizianzisha Biashara hizo kwa sababu tu wameona wengine wameanzisha.
2. Ni aina gani ya Biashara natakiwa
kufanya?
Sio kila Biashara unayoiona
inafanywa na wengine basi ukadhani kuwa nawe unaweza kuifanya. Ni lazima ujue
ni aina gani ya biashara unaweza kuifanya kulingana na kiasi cha mtaji
ulichonacho, taaluma, wafanyakazi n.k. Hivyo ni lazima ujiulize vizuri juu ya
aina ya Biashara unayotakiwa kuifanya.
3. Je Biashara hiyo ina
wateja?
Dhumuni kuu la Uanzishwaji wa
Biashara ni Kuuza ambapo mnunuzi ni Mteja. Hii ina maana kwamba kama Biashara
unayoanzisha haitakuwa na wateja (wa kutosha) basi hutaweza kufanya vizuri
kwenye Biashara hiyo. Hivyo ni vizuri mtu kuangalia kama Biashara yako
unayotaka kuanzisha ina wateja wa kutosha au la.
4. Ni bidhaa ipi au huduma gani
itakuwa kuu kwenye Biashara yangu?
Ni lazima ujue ni Bidhaa ipi (au
hutuma gani) itabeba biashara yangu. Mfano mfugaji wa kuku wa nyama, bidhaa
yake kuu ni kuku mwenyewe ingawa anaweza kuuza Mbolea inayotokana na kinyesi
cha kuku. Hivyo ni muhimu ujue kipi kitabeba Biashara yako.
5. Nina muda wa kutosha kusimamia
Biashara hiyo?
Biashara yoyote inahitaji muda wa
usimamizi na ufuatiliaji. Wengi wamekuwa wakifeli kwenye biashara zao kutokana
na kuanzisha Biashara halafu kuwaachia wengine wawaangalizie huku wao wenyewe
wakiwa aidha na muda mchache au kutokuwa na muda wa kufuatilia maendeleo ya
biashara zao. Hivyo ni vizuri kujiuliza kama utakuwa na muda wa kutosha wa
kufuatilia Biashara hiyo unayotaka kuanzisha.
6. Kipi kitakachotofautisha Biashara
yako na Biashara zingine?
Biashara inahitaji ubunifu na
upekee katika uanzishwaji wake. Kwenye Biashara unayotaka kuianzisha hautakuwa
peke yako. Ni lazima watakuwepo watu wengine wanaofanya biashara hiyo. Hivyo ni
lazima ujiulize ikiwa utaanzisha biashara hiyo, ni vitu gani vitakavyoweza
kutofautisha Biashara yako na Biashara za watu wengine.
7. Ni sehemu gani nzuri ya Kuiweka
Biashara hiyo?
Location! Location! Location! (Sehemu! Sehemu! Sehemu!) ndio maneno yanayopendwa kutumiwa (kwa
kurudiwa mara tatu) na wataalamu na washauri wa masuala ya kibiashara kuonyesha
umuhimu wa sehemu ya kufanyia Biashara. Ni lazima ujue sehemu nzuri ambayo
itaweza kufikiwa kwa urahisi na wateja ya kuweka Biashara yako. Pia ni vizuri
kuangalia sehemu ambayo inafikiwa na huduma za kijamii kama vile maji, umeme,
n.k. Uteuzi mbovu wa sehemu ya kufanyia biashara unaweza kufanya Biashara yako
iwe ni yenye kuleta hasara na kushindwa kuendelea Daima.
8. Nahitaji wafanya kazi wangapi
kwenye Biashara yangu?
Hili linategemea na ukubwa wa
biashara. Sio Biashara zote zitahitaji wafanyakazi. Zipo nyingine zitahitaji
uwepo wako tu. Hivyo kama biashara yako itahitaji wafanyakazi, ni vizuri kujua
ni wafanyakazi wangapi wanaohitajika. Hili litakusaidia kuweka vizuri bajeti
yako uanzishwaji wa Biashara.
9. Kuna mfanyabiashara mwingine
(Supplier) namuhitaji kwenye Biashara yangu?
Biashara huwa zinategemeana.
Unaweza ukawa ni muuzaji na katika muda huo huo unaweza kuwa ni mnunuaji. Hivyo
ni lazima ujue ni watu gani utakuwa unanunua vitu kwao ili kuendesha Biashara
yako. Mfano Mkulima mbali na kuuza mazao ila pia atahitaji Pembejeo za kilimo,
dawa n.k. kutoka kwa wafanyabishara wengine
10. Ni kiasi gani cha pesa nahitaji ili
Kuanza Biashara yangu?
Naam! Ni lazima uwe na kiasi cha
pesa kitakachotumika kama mtaji wa kuanzia katika biashara yako (Start Up
Capital). Hivyo baada ya kujua aina ya biashara unayotaka kufanya ni lazima pia
ujue mtaji wake. Usianzishe Biashara ambayo inahitaji kiasi cha mtaji ambacho
wewe huna au huwezi kukifikia. Wengi wamefeli kutokana na hili.
11. Ni njia gani nzuri ya kutumia ili
kupata Mtaji?
Zipo njia nyingi anazoweza kutumia
mtu ili kupata mtaji wa biashara yake. Kujiwekea Akiba, kukusanya pesa kutoka
kwa ndugu na marafiki, kukopa (Sio
mkopo wenye Riba), kuwekeza
faida (Retained earnings) ni miongoni mwa njia zinazoweza kutumika ili kupata
mtaji. Hivyo ni muhimu na vizuri kujua njia utakazotumia ili kupata mtaji wa
Biashara unayotaka kuanzisha.
12. Itanichukua muda gani mpaka
kukahakikisha Bidhaa yangu inawafikia wateja?
Hili ni swali ambalo wengi huwa
hawajiulizi. Umuhimu wa swali hili ni kuwa litakusaidia kwenye kupanga matumizi
mazuri kwenye Biashara yako. Unaweza ukakuta mtu anaanzisha biashara ambayo
gharama za uendeshaji kwa mwezi ni Tshs
2,000,000 huku wateja
aliowafikia hawafikishi hata mauzo ya Tshs
500,000. Huyu lazima
atashindwa kuendelea na Biashara yake. Hivyo ni muhimu kujua muda utakaotumia
kuwafikia wateja na kiasi utakachoingiza kwa muda huo.
13. Itanichukua muda gani hadi kuanza
kuiona faida ya Biashara yangu?
Lengo kuu la mtu kuanzisha Biashara
ni kupata faida. Hivyo ni lazima ujue muda gani utatumika ili kuanza kupata
faida tangu uanzishe Biashara hiyo. Hii itakusaidia kujua Uhai wa Biashara yako
utakuwaje hapo mbeleni
14.
Ni nani wapinzani wangu kwenye Biashara?
Naam! Kama tulivyosema awali kuwa
Huwezi kuwa peke yako kwenye Biashara unayoianzisha. Hivyo ni lazima uwajue
wapinzani wako na mbinu wanazozitumia kwenye mauzo yao. Hii itakusaidia kubuni
njia nzuri za kuendesha Biashara yako zitakazofanya uwashinde kwa wepesi.
15. Ni kiasi gani cha bei au ubora wa
bidhaa (au huduma) zangu nifanye ili kuwashinda wapinzani wangu?
Bei ya Bidhaa ni kitu muhimu cha
kuzingatia kwenye uanzishwaji wa biashara. Sio lazima bei yako iwe chini ya
wapinzani wako ndio uweze kuuza. Bei ya bidhaa huwa inawekwa kutokana na ubora
wa bidhaa yako. Hivyo ni lazima uangalie bei na ubora ambavyo vitaweza kuwa
vizuri kuliko wapinzani wako.
16. Vipi nitafuata taratibu za kisheria
kwenye Biashara yangu?
Kila biashara inayoendeshwa ina
taratibu zake za kisheria kutokana na nchi na nchi. Hivyo ni lazima ujue
taratibu za kisheria zinazohitajika kwenye biashara yako na uzifuate ipasavyo.
Wengi wameshindwa kuendelea na biashara zao katika ubora wake kutokana na
kushindwa kufuata taratibu za kisheria zilizopo kwenye bishara zao.
17. Malipo ya kodi?
Kodi ni jambo la lazima katika
Biashara. Hivyo ni lazima ujue ni kiasi gani kinahitajika ili kueweza kulipa
kodi. Pia ujue ni taratibu gani za kufuata katika malipo yako hayo ya kodi.
18. Matangazo?
"Biashara Matangazo." Ni
msemo wa waswahili katika Biashara. Ni lazima ujiulize vipi utafanya matangazo
ya Biashara yako. Ni lazima ujue njia gani zitatumika kuwafanya watu wajue
biashara yako. Njia hizo ni vizuri zikawa na gharama nafuu na zenye kuleta Tija
katika Biashara yako.
19. Uongozi na Usimamizi?
Biashara inataka usimamizi mzuri na
uongozi wa kuiendesha Biashara hiyo. Ni lazima wapatikane watu makini na wenye
ari ya kutimiza majukumu yao. Ikiwa uongozi wa kwenye Biashara yako hautakuwa
madhubuti na usimamizi usipokuwa wenye kueleweka, basi biashara hiyo lazima
itafeli.
20. Inaruhusiwa kwenye Uislamu?
Hili ni swali la msingi sana kwa
mjasiriamali wa kiislamu. Ni lazima ujue kama Biashara yako inaruhusiwa au
hairuhusiwi kufanywa kwa mujibu wa Uislamu. Unaweza kuomba ushauri kwa
wataalamu wa masuala ya dini na wakakujibu juu ya uhalali na uharamu wa
Biashara unayotaka kuanzisha.
HITIMISHO :
Usiwe na Pupa ya kuanzisha biashara bila ya kufanya utafiti wa
kutosha juu ya biashara hiyo. Ni lazima utengeneza mpango mzuri wa biashara
yako kama unahitaji biashara hiyo iwe ni yenye kukufikisha mbali Insha Allah.
Maassalaam.
No comments:
Post a Comment