Friday 22 July 2016

MAMBO 16 YA KUFANYA KWENYE UJANA



Amesema mtume Muhammad (Rah’ma na amani) kuwa hatoinua mja mguu wake siku ya Qiyama mpaka aulizwe juu ya mambo manne. Moja ya mambo hayo ni kuhusiana na ujana ambapo mja ataulizwa “Ujana wake aliutumia vipi.”

Wengi wetu tumefanya ujana ni umri wa mtu kujiachia na kufanya majambo ambayo hayana msingi kwenye maisha yetu ya Duniani na hata Akhera pia. Ni lazima tukubali kuwa dunia imebadilika. Dunia ya sasa sio ile ya zamani ya kuuchezea ujana kwa kuamini kuwa uzeeni utafanya mambo uliyoyakusudia.
Yafuatayo ni mambo 15 ya kufanya kabla ya kupita umri wa ujana wako ambao mara nyingi ni miaka kati ya 30 hadi 35.

1.  Maliza Masomo Yako.
Ni vizuri mtu akamaliza masomo yake kabla ya kupita umri wa ujana wake. Wameeleza wana sayansi kuwa umri chini ya miaka 30 ni umri ambao mtu akili yake inakuwa ni yenye nguvu na uwezo wake wa kujifunza mambo unakuwa ni wa haraka.

Hivyo ni vizuri kijana kuutumia umri huu kumaliza masomo yake na kuhakikisha anapata taaluma (Profession) atakayoitumia maishani mwake hasa sehemu za kazi maana hata kazi nazo siku hizi mbali na kuangalia taaluma pia unaangaliwa umri.

2.  Jifunze Fani Mbalimbali.
Mbali na taaluma uliyoipata shuleni ni vizuri ukajifunza fani walau mbili tatu kutoka kwenye mafunzo ya ufundi stadi. Unaweza kujifunza udereva, ufundi ujenzi, ufundi seremala, ufundi cherehani n.k. Fani hizi zitakusaidia sana maishani mwako aidha kwa shughuli zako binafsi au hata kwa shughuli za kukuingizia kipato.

3.  Jifunze stadi za maisha.
Kuna mengi ya kujifunza maishani mwetu. Mfumo wetu wa elimu umeweka mbali sana mafunzo ya stadi za maisha. Kutokana na umuhimu wake mkubwa maishani mwetu, ni lazima kujifunza majambo haya. Vitu kama kupika, kufua, na kazi zingine za nyumbani ni vizuri mtu akajifunza katika ujana wake. Vilevile kujifunza kuhusu mahusiano, maisha katika jamii n.k ni mambo yanayoshauriwa sana mtu ajifunze katika ujana wake.

4.  Jifunzi Dini yako.
Mfumo wa maisha ya mwanaadamu wenye kuelekeza zuri na baya, la kufanya na la kutofanya, upo ndani ya dini.

Maisha kiujumla wake yamejaa mengi. Maisha yamejumuisha mambo mazuri na pia yamejumuisha mambo mabaya. Ni vizuri mtu akautumia umri wake wa ujana vilevile kujifunza dini yake. Ajue kusoma kitabu cha Mola wake na vilevile ajue mambo yote ya msingi yanayohusiana na dini yake.

5.  Ijue Historia ya Familia na Ukoo wako.
Hakuna kitu kizuri maishani kama kuijua familia yako na ukoo wako kwa ujumla wake. Jua wapi wazazi wako walipotokea. Jua baba na mama zako wadogo kwa majina na mahala wanapoishi. Wajue wajomba, mashangazi, makaka, madada na wote wanaoihusu familia yako.

Hii itatengeneza mahusiano mazuri kati yako na familia yako kiujumla na kupanga mikakati mizuri ya kusaidiana inapotokea shida. Pia itakusaidia kujua nani anaweza kushirikiana nawe katika harakati za kimaendeleo.

6.  Anza kuweka akiba.
Chukua mfano wa kijana mwenye umri wa miaka 15. Akisema kila siku aweke Tshs 1,000/=, maana yake kwa mwezi anauwezo wa kuwa na Tshs 30,000/= ambapo kwa mwaka anakuwa na Tshs 360,000/=. Kama tukisema twende hadi miaka 30, kijana huyu atajikuta ana Tshs 5,400,000/=.

Hicho ni kiasi kikubwa sana ambapo mtu anaweza kusema anunue kiwanja, aanze biashara, au awekeze popote atakapo. Ila yote hiyo itatokana na kuweka akiba.

Ni vizuri mtu akawa na utaratibu wa kuweka akiba kwenye ujana wake walau unapofikia umri wa uzeeni basi unakuwa na kiasi cha kukusaidia kuendesha maisha yako.

7.  Anza kufanya kazi na anzisha kazi zako Binafsi.
Naam! Kazi ndio msingi mkubwa katika kuendesha maisha yetu ya kila siku. Iwe kazi ya kuajiriwa au kujiajiri, basi hakikisha unakuwa na kazi kabla ya kupita kwa umri huo.

Kazi yoyote ya halali ikifanywa vizuri, na kwa Ari basi inaweza kuleta tija kubwa katika maisha ya mtu.

Jitahidi kupata kazi ya halali itakayokuingizia kipato cha halali kabla ya kupitwa na ujana wako kwani wapo wazee wengi wanahadhirika maishani mwao kwa kushindwa kupata cha kujishughulisha nacho ujanani mwao.

8.  Kuwa na utaratibu wa kujisomea.
Alisema msomi mmoja kuwa, ukitaka kumfichia kitu mu Afrika, basi muwekee kwenye ktabu. Hii ina maana kuwa wa Afrika wengi, watanzania tukiwemo, hatuna utaratibu wa kujisomea.

Kwenye kujisomea kuna faida nyingi. Mbali na kufanya akili kuwa safi muda wote pia mtu anapata wasaa wa kujifunza vitu vipya ambavyo vinaweza kumsaidia maishani mwake kwa sasa na baadae pia.

Ni vizuri ukajiwekea utaratibu wa kujisomea vitabu, makala, magazeti n.k kuhusiana na masuala ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara na mambo mengine yanayohusu maisha.

9.  Jiunge na vikundi vya kijamii.
Kuna msaada mkubwa sana mtu kuwa kwenye vikundi vinavyofanya kazi za kuhudumia jamii. Vipo vikundi vya kifedha, michezo na utamaduni, afya, dini na vingine vingi. Ndani ya vikundi hivi unaweza kukutana na watu wapya mnaoweza kusaidiana katika maisha pia unaweza kutumia kama njia moja wapo ya kusaidia jamii inayokuzunguka.

10.    Acha! Acha! Acha! – Kuvuta Sigara, Ulevi, Uzinifu.
Asilimia kubwa ya vijana hupenda kuvuta sigara, ulevi na hata uzinifu. Kwa sasa huenda usiyaone madhara yake kwani ni vitu ambavyo huwa vinakula taratibu taratibu. Ila kwa miaka ya mbeleni unaweza kuja kukutana na madhara makubwa ambayo yanaweza kukufanya upoteze furaha ya maisha yako.

Jitahidi sana katika ujana wako kuojihusisha na uvutaji wa sigara, ulevi na uzinifu pia kwani gharama zake mbeleni ni kubwa mno.

11.    Funga ndoa.
Naam! Jitahidi sana kufunga ndoa kabla ya kupitwa na ujana wako. Mbali na kupata utulivu wa nafsi, ila itasaidia kuongeza uwajibikaji na umakini kwenye mambo mbalimbali ya maisha yako. Pia itasaidia kupata watoto mapema ambao wanaweza kuja kukusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yako ya mbeleni hasa katika shughuli zako za kila siku na Biashara zako kwa ujumla.

Kubwa ni kuheshimika katika jamii kwani asilimia kubwa ya watu waliopo kwenye ndoa huwa wanapewa heshima kubwa kwenye jamii zao na kushirikishwa kwenye baadhi ya majambo ya msingi.

12.    Kuwa na Ratiba.
Ni kawaida sana katika zama zetu kumkuta kijana hana jambo la kufanya. Yaani ukimkurupua kumwambia akusindikize sehemu, basi atakwenda muda huo huo na ukimuuliza huna la kufanya atakujibu ndio.

Ni vizuri kijana akapanga muda wake na kupanga mambo yake ya siku nzima. Jifunze kuweka ratiba ya kufanya mambo yako ya siku, wiki, mwezi na hata mwaka pia. Hii itakusaidia kufikia malengo yako ki urahisi na kutopata muda wa kufanya vitu visivyo na msaada maishani mwako.

13.    Tengeneza Mtandao wa watu watakaokusaidia. baadae
Kwa lugha ya kiingereza wanasema “Networking.” Jitahidi kuwa na network nzuri, yenye watu wazuri na wenye manufaa maishani mwako. Hakikisha kila mtu mzuri unayekutana nae unatengeneza nae mahusiano mazuri yatakayokunufaisha wewe na kumnufaisha yeye pia.

Hakikisha unapata marafiki kwenye kila idara ya kiuchumi, siasa, utamaduni na masuala ya kijamii pia.

14.    Mazoezi! Mazoezi! Mazoezi.
Hili ni jambo la msingi sana kwa kijana. Hakikisha unakuwa ni mwenye kufanya mazoezi walau mara mbili kwa wiki. Chagua mazoezi yatakayoendana na muda wako wa kazi na muda wako wa mambo mengine. Ni vizuri kufanya mazoezi asubuhi au/na jioni. Hii itasaidia kuuweka mwili wako vizuri na wenye afya muda wote. Vilevile itasaidia kukuweka mbali na magonjwa madogo madogo yanayoweza kupunguza ufanisi kwenye shuguli zako.

15.    Jifunze Lugha za Kigeni.
Dunia ya leo ni dunia ya utandawazi. Watu kutoka mataifa mbalimbali wanawekeza kwenye nchi za wengine. Ni vizuri ukajifunza lugha za kigeni hasa za mataifa yanayokuja kuwekeza kwenye nchi yako. Lugha itatanua wigo wako wa ajira, biashara, na hata kujua tamaduni za watu wengine.

16.    Jiweke mbali na madeni.

Hakuna kitu kinachorudisha nyuma watu kama vile madeni. Madeni humfanya mtu kila kipato anachopata kina kwenda kulipa madeni na badala ya kufanya maendeleo ya maisha yake. Hivyo jitahidi sana kuepuka madeni ndani ya umri huu. Kama kuna watu au taasisi inakudai basi fanya juu chini kulipa madeni hayo haraka na epuka kwa hali na mali kukopa (hasa mikopo yenye riba).

No comments:

Post a Comment