·
Maana Ya Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni zaka au sadaka ya lazima inayotolewa baada ya
kumalizika Ramadhani, na kuingia tarehe mosi ya mwezi Shawwali (Mfungo Mosi). Imeitwa
Zakatul – Fitri kwa sababu ni Zaka inayotolewa baada ya kufuturu (kumaliza
Wajibu wa kufunga Ramadhani).
Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbas (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe
Juu Yake) “Zaka ya Fiti ni kitakaso cha aliyefunga kutokana na mambo ya upuuzi
na maneno machafu, na ni Lishe kwa masikini. Hivyo, atayeitoa kabla ya Swala,
basi itapokewa kama Zaka, na ataye itoa baada ya Swala basi ni sadaka kama
sadaka yoyote ile nyengine.”
Wanachuoni wa Fiqh, huielezea na Zaka ya Fitri kwamba: “ Zaka ya
Fitri ni Sadaka ya uwajibu maalumu, ya kiwango maalumu, kutoka kwa mtu maalumu
, kwa masharti maalumu, kwa niaba ya watu maalumu, kupewa watu maalumu; kwa
lengo maalumu; nalo ni Kikataso cha Swaumu na Chakula kwa masikini.”
Zaka ya Firi imefaradhishwa mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili
Hijriyya, kama kitakaso cha mwenye kufunga Ramadhani.
·
Wanaolazimikiwa Na Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni wajibu kwa kila nafsi Mwislamu aliyehai. Ni
Zaka ya kiwiliwili, si zaka ya mali. Hivyo, midhali kiwiliwili kipo basi lazima
kitolewe zaka ya Fitri. Ni wajibu. Ni Faradhi. Haiepukiki, isipokuwa kwa yule
ambaye hana uwezo kabisa.
Ama mwenye kipato, au mwenye wajibu wa kumtunza mtu mwengine,
kama mke, watoto, Wazee wake wawili wasiojiweza, watumishi wa nyumbani na
kadhalika, na kipato chake kikawa kinazidi wajibu wake wa kuwatunza anaowatunza,
basi ni wajibu kwake kujitolea yeye mwenyewe, kwanza, na kisha kuwatolea wote
wale anaowajibika kuwatunza, kwa hali na mali. Yaani, lazima awe na chakula cha
ziada ya kula yeye na familia yake, siku ya Idi.
Hicho kitachozidi ndicho kinachotolewa Zaka ya fitri. Kikiwa
hakitosho kulisha family yake hiyo, siku ya Idi, basi hana jukumu la kutoa Zaka
ya Fitri.
Kwa maneno mengine, iwapo baba mwenye nyumba ni masikini, hana
cha kumtosha yeye na familia yake siku ya Idi, basi huyo hana wajibu wa kutoa
zaka ya Fitri. Wala hana wajibu wa kumtolea mkewe, hata kama mke huyo ni mwenye
uwezo kutokana na kipato chake mwenyewe.
Lakini mke, mwenye kipato chake mwenyewe, anaweza kujitolea
kumtolea mumewe na watoto wake akipenda. Maana hana wajibu wa kujitunza, wala
kumtunza mumewe wala watoto wake. Ni hiari yake, na ni fadhila kubwa, sana,
kufanya hivyo. Ila SI wajibu juu yake.
·
Vinavyopaswa Kutolewa Kwenye Zakatul – Fitri na Viwango Vyake.
Kinachotakiwa Kutolewa kwenye Zakatul - Fitri ni chakula, na
wala sio pesa. Na kiwango cha kutolewa ni pishi moja ya chakula kinacholiwa
sana katika jamii husika. Hivyo, vyakula vinavyo ingia hapa ni nafaka zote,
kuanzia ngano, shayiri, mchele, unga wa ngano, sembe, maharage, ulezi, na
kadhalika. Ni chakula kinacholiwa sana na watu wengi katika jamii ya mtoa Zaka
hiyo.
Kiwango cha Zaka ya Fiti ni Pishi moja, ambayo ni sawa na kilo
mbili na grm 400; kwa pishi ya Mtume ﷺ (Pishi ya Mtume ﷺ ni sawa na vibaba vine, vya Mtume ﷺ . Na kibaba kimoja ni ujazo wa nafaka
kwenye viganja viwili kwa pamoja vya mtu wa kawaida.) Hivyo, ni kama kilo mbili
na nusu za chakula kinachopendwa sana na jamii husika. Kiwango hicho ni kwa
kila kiumbe, chenye uwezo wa kujitolea chenyewe.
·
Yakuzingatia Katika Utoaji wa Zakatul - Fitri
1.
Kuitoa mara baada ya kuandama mwezi wa Shawwal: yaani usiku wa
kuamkia Siku Kuu, au kabla ya kwenda kuswali Swala ya Idi. Au kabla ya siku
moja au mbili ya kumalizika Ramadhani.
2. Kumtolea hata mtoto aliyetumboni,
kama alivyokuwa akifanya Sayyidina Uthman bin ‘Affan رضي
الله عنه . Ameipokea Ahmad na
Ibn Abi Shayba.
3. Kuigawa kwa mikono yako,
mwenyewe, badala ya kuwapa watu wengine waitoe kwa niaba yako. Mtume ﷺ akifanya hivyo, na kuwausia Maswahaba nao
wafanye hivyo.
4. Ukiwapa watoto wako nyumbani
kuitoa, ni sawa na kuigawa mwenyewe.
5. Kuwapa masikini jamaa zako, wenye
kustahiki na ambao huna wajibu wa kuwatunza.
6. Kuigawa kwa masikini wa mahali
ulipo, ila ikiwa kuna wanaohitaji zaidi, na ni jamaa zako, nchi nyengine.
7. Iwapo chakula unachotoa kina
viwango mbali mbali, basi chagua kiwango cha juu: Mwenyezi Mungu amesema:
“Hamtaipata Pepo mpaka mtoe mnavyo vipenda.”
8. Kutoa nafaka kavu, inayoweza
kuhifadhika kwa siku kadhaa bila ya kuharibika, ni bora kuliko chakula
kisichoweza kuhifadhika kwa muda mrefu.
9. Kwa upande wa Wazazi wako wawili,
basi sunna kumtolea Mama mzazi kwanza, kisha ndiyo Baba mzazi – iwapo
wanakutegemea kuwatunza.
10.
Kuwapa majirani zako masikini, ni bora kuliko masikini wa mbali.
Imechukuliwa kutoka katika Post ya Shaykh Shareef Abdulqader
No comments:
Post a Comment