Imeandikwa katika Historia kuwa, wafanyabiashara wakubwa katika
zama zilizopita hasa kwenye ukanda wa Mashariki ya kati ya dunia (Middle East)
walikuwa ni Waislamu. Wao walizifanya shughuli zao za kiujasriamali kama Ibada
na ni moja ya njia za kueneza dini na kutengeneza jamii yenye tabia njema
iliyojaa uaminifu na uadilifu pia. Waliweza kufikia kilele cha juu kabisa cha
maadili katika shughuli zao. Kwa ufupi tunaweza kusema, walikuwa ni
wajasiriamali waliofanikiwa (Duniani na Akehra) jambo ambalo wajasiriamali wa
karne hii ya 21 wamelipoteza
Zifuatazo ni hatua 11 za kuelea Ujasiriamlai wenye Mafanikio.
1.
Kuwa na Ikhalas.
Imesemwa katika Hadithi kuwa Matendo hulipwa kutokana na nia na
kila mtu atalipwa matendo yake kulingana na nia aliyoiweka kwenye matendo hayo.
Ifanye Biashara yako kama ni moja ya sehemu ya kupata Radhi za Mwenyezi Mungu.
Kuwa na Ikhlas ndani yake na uifanye kwa kutegemea kuwa Allah atakulipa malipo
yaliyo ya kheri kutokana na biashara hiyo.
2.
Fanya Istikhara.
Istikhara ni kumuomba Mwenyezi Mungu ushauri na ukupe maamuzi
yaliyo na kheri nawe kwenye jambo linalokutatiza. Allah ndiye nayetujua zaidi
kuliko tunavyojiujua sisi wenyewe. Ni vizuri kufanya Istikhara kabla ya kuanza
biashara zetu na kumuomba Allah akupe yaliyo na kheri kwenye biashara yako
hiyo. Jifunze Jinsi ya Kuswali swala ya istikhara hapa.
3.
Fanya Shura.
Mwenyezi Mungu amewasifu waumini kwa sifa ya kufanya majambo yao na
kuyapeleka kwa mfumo wa “Shura” (42:38). Shura ni kutafuta ushauri na maoni juu
ya jambo Fulani kutoka kwa watu wengine. Ni vizuri ukapata ushauri juu ya
Biashara yako kutoka kwa wataalamu waliobobea na wenye kuaminika kulingana na
bishara uliyonayo.
4.
Jielimishe.
Moja kati ya Sifa za Mjasiriamali wa Kiislamu ni kupenda kujielimisha. Kujielimisha huku kunatakiwa kuanzie mwanzoni na
kuendelea nako kwenye mchakato mzima wa kuelekea bishara yenye mafanikio.
Jielimishe kupitia Vitabu sahihi vinavyohusu Biashara yako, hudhuria semina na
ikiwezekana jiunge na kozi mbalimbali zitakazokusaidia kuwa madhubuti kwenye
Biashara yako.
5.
Angalia Mtaji Wako.
Moja kati ya maswali ya kujiuliza mjasiriamali akiwa kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ni mtaji wake. Ni
lazima ajue anahitaji kiasi gani cha mtaji na wapi atapata mtaji huo. Ni vizuri
kwa mjasiriamali wa kiislamu ahakikishe biashara yake inaanzishwa na mtaji wa
halali na anaouridhia Mwenyezi Mungu. Pia ni lazima aanzishe biashara
inayoendana na mtaji wake na achunge mtaji huo usije ukapotea kizembezembe.
6.
Angalia Fursa Zilizopo.
Usije kuanzisha Biashara ambayo sio Fursa kwani huenda ukakosa
muendelezo mzuri wa biashara hiyo. Ni lazima uangalie Fursa zilizopo ndani ya
biashara unayotaka kuanzisha na hata nje ya biashara yako hiyo. Angalia fur’sa
za halali na zenye kuleta tija katika jamii inayokuzunguka.
7.
Weka Ratiba Madhubuti.
Si katika maisha ya kila siku tu, hata kwenye masuala ya
ujasiriamali, suala la ratiba lina umuhimu mkubwa sana. Sio Ratiba tu ilimradi
ratiba, ila ni ratiba madhubuti. Hakikisha unaandaa ratiba nzuri ya shughuli
zako kwa kuzingatia masuala ya kiibada, kijamii, kiafya n.k
8.
Simamia Malengo Yako.
Mafanikio ya kwenye maisha yako ya duniani na akhera yapo kwenye
mikono yako mwenyewe. Ukiwa kama mjasiriamali wa kiislamu ni lazima uhakikishe
unasimamia malengo yako uliyojiwekea. Usikubali kuyumbishwa (bila sababu ya
msingi). Kila siku kabla ya kulala ni lazima ujifanyie hesabu ni kwa kiasi gani
umeyafikia malengo uliyoyakusudia, na kila unapoamka lazima ujiwekee njia
utakazotumia kwa siku hiyo kuyafikia malengo hayo.
9.
Tengeneza Mtandao wenye Manufaa.
Hakuna jambo zuri kwenye maisha na kwenye ujasiriamali (hasa wa
kiislamu) kama mtu kuwa na mtandao wenye manufaa. Hakikisha unazungukwa na watu
ambao watakusaidia kwa namna moja ama nyingine kufikia malengo uliyoyakusudia.
Hakikisha unakuwa na mawasiliano yao ya simu, barua pepe (email), na kujua
sehemu zao za kazi na vipi wataweza kukusaidia kwenye kutimiza malengo yako.
10.
Jifunze Kutokana na Makosa.
Asilimia kubwa ya watu wasiojifunza kutokana na makosa (aidha
waliyoyafanya wao au yaliyofanywa na wengine) huwa wana tabia ya kurudia makosa
yaleyale. Kama mjasiriamali wa kiislamu ni lazima ujue ulipokosea na uweke
mikakati madhubuti ya kutorudia tena makosa hayo.
11.
Safisha Mali Zako.
Naam usafi wa mali ni jambo la muhimu sana kwa mjasiriamali wa
kiislamu. Jambo hili limesahaulika mno na wajasiriamali wengi wa kiislamu. Njia
kuu ya kusafisha mali zako ni kwa Kutoka zaka (kama kiwango cha mali zako
kinafikia kutoa zaka). Njia zingine ni kutoa sadaka, kusaidia wanafunzi malipo
yao ya masomo, kusaidia masikini n.k
Kwa Muislamu, Ujasiriamali ni sehemu ya Ibada na ni moja ya njia
zinazoweza kutumika kuufikisha uislamu katika ubora wake. Ni vizuri tukawa na
malengo makubwa ya kufanya shughuli zetu za kiujasiriamali ni zenye kufanikiwa
kwa kufuata kanuni na sheria zilizopo kwenye uislamu insha allah.
Maassalaam.
No comments:
Post a Comment