
KIWANDA cha Sukari cha Manyara (Manyara Sugar)
kilichopo katika kijiji cha Matufa wilayani Babati mkoani Manyara, kimeiomba
Halmashauri ya Wilaya ya Babati kusaidia kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima
kulima miwa kwa wingi kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Meneja wa kiwanda hicho, Pratap Disodya
aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kiwanda hicho hakina sababu ya kuficha
sukari kwa kuwa kina uwezo wa kuzalisha tani 300 hadi 500 kwa siku.
Alisema pamoja na uzalishaji huo unaochangiwa
na upungufu wa miwa kutoka kwa wakulima, kiwanda hicho pia kinalazimika
kufungwa kila mwaka ifikapo Desemba hadi Juni kusubiri uzalishaji uanze Juni.
Alisema katika kuitikia agizo la Rais John
Magufuli la kuwataka wafanyabiashara wote walioficha sukari katika maghala yao
kuanza kusambaza mara moja vinginevyo serikali itachukua hatua kali, kiwanda
hicho kimethibitisha kutokuwa na akiba ya kutosha ya sukari inayozalishwa
kiwandani hapo.
Alisema wakulima wakihimizwa kuzalisha miwa kwa
wingi uzalishaji utaongezeka na kupunguza uhaba wa sukari nchini. Disodya
alisema tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho mwaka 2005 na kuanza uzalishaji
mwaka 2007, kimezalisha tani 150 mwaka 2013 pekee.
Alisema hatua walizochukua ni pamoja na uongozi
wa kiwanda kuendelea kuwahamasisha wakulima wadogo zaidi ya 1,500 kuongeza
uzalishaji wa miwa kwa kuwapatia mikopo.
Chanzo : Tovuti ya Habari Leo
No comments:
Post a Comment