Saturday 30 April 2016

SIFA ZA MJASIRIAMALI WA KIISLAMU.



Kuna Tofauti kubwa sana kati ya wajasiriamali wa kiislamu na wajasiriamali wengine. Tofauti hiyo inatokana na ukweli kwamba, wajasiriamali wa kiislamu huendesha shughuli zao za kijasiriamali za kila siku kwa kutumia Quran na Sunna kama msingi mkuu na muongozo mkuu wa uendeshaji wa shughuli zao za kiujasiriamali.

Vilevile ni Muhimu Kujua kwamba sio kila mjasiriamali ambaye ni muislamu ana sifa za kuwa mjasiriamali wa kiislamu.

Zifuatazo ni sifa za Mjasiriamali wa Kiislamu;

1.       Taqwa.
Kumuogopa Mwenyezi Mungu (Taqwa) ndio sifa ya kwanza ya Mjasiriamali wa kiislamu. Hii ina maana kwamba, kuanzia kwenye kupata wazo la kufanya Biashara hadi kwenye kuifanya biashara yenyewe, Mjasiriamali wa kiislamu anakuwa ni mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu. Anakuwa ni mwenye kuhakikisha Biashara yake inafuata kanuni na taratibu za uendeshaji Biashara kwa mujibu wa Uislamu.

2.       Chumo la Halali.
Mjasiriamali wa kiislamu anahakikisha chumo lake ni la halali muda wote. Kuanzia pesa yake ya mtaji wa Biashara hadi kwenye faida ya biashara yake, anahakikisha uhalali mkubwa unakuwepo ndani ya Biashara yake. Haruhusu kuingizwa kwa chumo la Haramu ndani ya Biashara yake.

3.       Kujiweka Mbali na Israfu.
Israfu (Kusaza) ni jambo ambalo Mjasiriamali wa kiislamu hujiepusha nalo muda wote. Israfu kwenye Biashara huja pale ambapo mtu anafanya Biashara bila mahesabu mazuri. Anafanya matumizi hovyo hovyo bila mpangilio maalumu. Pia israfu yaweza kuja hata kwa mtu kumiliki mali nyingi mno kiasi cha kwamba wengine wanashindwa kutumia fursa zinazojitokeza kutokana na umiliki wake huo. Hana habari ya kupunguzia wengine wala kuwawezesha. Ila kwa mjasiiriamali wa kiislamu sifa hii hana na hujiweka mbali na israfu.

4.       Ibada
Naam ! ! ! Ibada ndio msingi mkuu wa maisha ya muislamu. Mjasiriamali wa kiislamu ibada kwake huja kwanza kisha mengine hufuata. Ibada kama vile swala huwa haimpiti na wala Biashara yake hamzuii kuswali. Kutoa Zaka, Swadaqa, Kufunga Ramadhan, kusoma Quran n.k. ni ibada ambazo mjasiriamali wa kiislamu huzipa kipaumbele katika maisha yake.

5.       Tabia Njema
Mjasiriamali wa kiislamu hudumu na tabia njema muda wake wote. Kusema ukweli, ukarimu, upole, kusaidia wengine ni miongoni mwa tabia njema anazojipamba nazo mjasiriamali wa kiislamu.

6.       Uaminifu
Uaminifu ni sifa nyingine nzuri ya mjasiriamali wa kiislamu. Si mdhulumati na wala si mtu wa kughushi kwenye Biashara zake. Huendesha Biashara zake kwa uaminifu wa hali ya juu kuanzia kwa washikadau (Shareholders) hadi kwa wateja wake (Customers).

7.       Kuzingatia wajibu wake kwenye Jamii.
Kila mjasiriamali ana wajibu katika jamii yake (Social Responsibility). Mjasiamali wa kiislamu huzingatia wajibu wake kwa jamii kama vile kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kwa hali na mali. Wajibu mkubwa walionao wajisiriamali wa kiislamu ni kutoa Zaka na kuhakikisha mambo ya afya, elimu n.k. yanaenda vizuri katika jamii zao.

8.       Kupenda Kujifunza.
Kujifunza (na kutafuta maarifa) ni jambo ambalo limesisitizwa kwa waislamu wote kwa ujumla wake. Vilevile uendeshaji wa shughuli za kiujasiriamali unataka mtu awe ni mwenye kujifunza vitu mara kwa mara. Mbali na kupenda kujifunza mas’ala yanayohusu dini, pia mjasiriamali wa kiislamu ni mwenye kupenda kujifunza kuhusu masuala ya kibiashara na ni mwenye kuendana na mabadiliko ya soko na hali ya kiuchumi kila siku.
  

Hizo ndizo sifa 8 kuu za mjasiriamali wa kiislamu. Tjuitahidi kujipamba na sifa hizo na Insha Allah mafanikio yataonekana kwenye shughuli zetu za kijasiriamali . . . Aaamin.

No comments:

Post a Comment