Monday 25 July 2016

VITU VINNE VITAKAVYOFANYA BIASHARA YAKO ITHAMINIWE


Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusiana na wateja kudharau biashara zao au hata kutopata wateja wanaothamini biashara zao. Hii inatokana na sababu kadhaa ambazo huenda zikawa upande wa mfanyabishara au hata mteja mwenye pia.

Kuna mambo kadhaa ambayomfanya biashara anatakiwa kuyafanya ili kuifanya biashara yake kuwa na thamani kwa wateja au hata watu wengine.

1.  Jina la Biashara.
Jina la Biashara yako ndio kitu cha kwanza kitakachowafanya wateja na watu wengine waithamini Biashara hiyo. Jina ni lazima liwe jepesi, fupi na lenye kuleta maana nzuri kwa wateja uliowakusudia na jamii kwa ujumla wake. Ni lazima uwe na jina la biashara litakaloendana na Biashara yako au kile unachokifanya kwenye shughuli zako za kila siku au hata jina litakaloakisi sekta unayofanyia kazi.

Uchaguzi mbovu wa jina unaweza kufanya watu wakaidharau biashara yako na wasiwe ni wenye kuitilia umakini. Vilevile kufanya Biashara ambayo haina jina kunaweza kusababisha ukose baadhi wa wateja ambao watahisi haupo serious na biashara yako.

2.  Machapisho.
Machapisho yana umuhimu mkubwa sana kwenye kumfanya mtu aithamini biashara yako. Mbali na kutumika kwenye kutangaza Biashara, pia machapicho yanaweza kutengeneza picha nzuri kwa mteja na kumfanya ahisi kuwa upo makini na unachokifanya.

Machapisho hayo yamejumuisha Vipeperushi, Business Cards, Mabango, Kalenda, Majarida, Vitabu, Fulana, n.k. Vilevile unaweza kuchapisha nembo ya biashara yako sehemu zingine kama vile kwenye kalamu, vikombe, au hata funguo.

Hii itafanya watu waithamini biashara yako katika thamani ya hali ya juu.

3.  Tovuti.
Tovuti hufahamika kwa urahisi kama “Website”. Katika dunia ya leo mtu anaposikia au kuona biashara yako na akavutiwa nayo, basi atakachofanya ni kuingia kwenye mtandao na kutafuta tovuti yako ili ajue unachokifanya kwa undani.

Hivyo asipoona tovuti yako kwenye mtandao hatoweza kufahamu unachokifanya na hii ndio itakuwa hatua ya kwanza ya mtu kutoithamini biashara yako.

Vilevile watu wengi inapowajia dhana ya kutaka kitu cha kununua huwa wanaanza kukitafuta kitu hicho kwenye mitandao. Hivyo utakapokosa tovuti nzuri yenye utalaamu wa kutosha, basi hakuna mtu atakayeweza kukufahamu na unaweza kukosa wateja wengi sana kwenye biashara yako.

Ni vizuri kwa mfanyabiashara kuwa na tovuti nzuri, yenye gharama nafuu, itakayoelezea biashara yake kwa ujumla na hata kuweka baadhi ya ripoti na mafanikio yanayohusiana na biashara yake hiyo.

4.  Barua pepe.
Huenda kikaonekana ni kitu kidogo sana, ila barua pepe (email) ni kitu cha muhimu sana kwenye biashara za kileo.

Wafanya biashara wengi katika zama zetu hupenda kutumia simu kwa kuwasiliana na wateja wao. Ila ni lazima tutambue kuwa watu wengi hupenda kuulizia biashara kupitia barua pepe na kueleza wanayoyahitaji pia. Hii hutengeneza mahusiano yako na mteja ambapo mkishajuana vizuri ndio hufuata mazungumzo ya njia ya simu.

Hivyo ni lazima kwa mjasiriamali wa kileo kuwa na barua pepe atakayotumia kuwasiliana na wateja wake.

Hakikisha unakuwa na barua pepe iliyokaa kiofisi zaidi. Usipende kutumia barua pepe zenye @gmail.com, @yahoo.com, @hotmail.com. Barua pepe za namna hii huwa hazileti mashiko na kwa wateja makini huenda ndio ikawa hatua ya kwanza ya kutothamini biashara yako. Tumia barua pepe zenye jina lako la biashara hasa ile itakayoendana na tovuti yako. Mfano marwa@tigo.com


Soma Zaidi »

Friday 22 July 2016

MAMBO 16 YA KUFANYA KWENYE UJANA



Amesema mtume Muhammad (Rah’ma na amani) kuwa hatoinua mja mguu wake siku ya Qiyama mpaka aulizwe juu ya mambo manne. Moja ya mambo hayo ni kuhusiana na ujana ambapo mja ataulizwa “Ujana wake aliutumia vipi.”

Wengi wetu tumefanya ujana ni umri wa mtu kujiachia na kufanya majambo ambayo hayana msingi kwenye maisha yetu ya Duniani na hata Akhera pia. Ni lazima tukubali kuwa dunia imebadilika. Dunia ya sasa sio ile ya zamani ya kuuchezea ujana kwa kuamini kuwa uzeeni utafanya mambo uliyoyakusudia.
Yafuatayo ni mambo 15 ya kufanya kabla ya kupita umri wa ujana wako ambao mara nyingi ni miaka kati ya 30 hadi 35.

1.  Maliza Masomo Yako.
Ni vizuri mtu akamaliza masomo yake kabla ya kupita umri wa ujana wake. Wameeleza wana sayansi kuwa umri chini ya miaka 30 ni umri ambao mtu akili yake inakuwa ni yenye nguvu na uwezo wake wa kujifunza mambo unakuwa ni wa haraka.

Hivyo ni vizuri kijana kuutumia umri huu kumaliza masomo yake na kuhakikisha anapata taaluma (Profession) atakayoitumia maishani mwake hasa sehemu za kazi maana hata kazi nazo siku hizi mbali na kuangalia taaluma pia unaangaliwa umri.

2.  Jifunze Fani Mbalimbali.
Mbali na taaluma uliyoipata shuleni ni vizuri ukajifunza fani walau mbili tatu kutoka kwenye mafunzo ya ufundi stadi. Unaweza kujifunza udereva, ufundi ujenzi, ufundi seremala, ufundi cherehani n.k. Fani hizi zitakusaidia sana maishani mwako aidha kwa shughuli zako binafsi au hata kwa shughuli za kukuingizia kipato.

3.  Jifunze stadi za maisha.
Kuna mengi ya kujifunza maishani mwetu. Mfumo wetu wa elimu umeweka mbali sana mafunzo ya stadi za maisha. Kutokana na umuhimu wake mkubwa maishani mwetu, ni lazima kujifunza majambo haya. Vitu kama kupika, kufua, na kazi zingine za nyumbani ni vizuri mtu akajifunza katika ujana wake. Vilevile kujifunza kuhusu mahusiano, maisha katika jamii n.k ni mambo yanayoshauriwa sana mtu ajifunze katika ujana wake.

4.  Jifunzi Dini yako.
Mfumo wa maisha ya mwanaadamu wenye kuelekeza zuri na baya, la kufanya na la kutofanya, upo ndani ya dini.

Maisha kiujumla wake yamejaa mengi. Maisha yamejumuisha mambo mazuri na pia yamejumuisha mambo mabaya. Ni vizuri mtu akautumia umri wake wa ujana vilevile kujifunza dini yake. Ajue kusoma kitabu cha Mola wake na vilevile ajue mambo yote ya msingi yanayohusiana na dini yake.

5.  Ijue Historia ya Familia na Ukoo wako.
Hakuna kitu kizuri maishani kama kuijua familia yako na ukoo wako kwa ujumla wake. Jua wapi wazazi wako walipotokea. Jua baba na mama zako wadogo kwa majina na mahala wanapoishi. Wajue wajomba, mashangazi, makaka, madada na wote wanaoihusu familia yako.

Hii itatengeneza mahusiano mazuri kati yako na familia yako kiujumla na kupanga mikakati mizuri ya kusaidiana inapotokea shida. Pia itakusaidia kujua nani anaweza kushirikiana nawe katika harakati za kimaendeleo.

6.  Anza kuweka akiba.
Chukua mfano wa kijana mwenye umri wa miaka 15. Akisema kila siku aweke Tshs 1,000/=, maana yake kwa mwezi anauwezo wa kuwa na Tshs 30,000/= ambapo kwa mwaka anakuwa na Tshs 360,000/=. Kama tukisema twende hadi miaka 30, kijana huyu atajikuta ana Tshs 5,400,000/=.

Hicho ni kiasi kikubwa sana ambapo mtu anaweza kusema anunue kiwanja, aanze biashara, au awekeze popote atakapo. Ila yote hiyo itatokana na kuweka akiba.

Ni vizuri mtu akawa na utaratibu wa kuweka akiba kwenye ujana wake walau unapofikia umri wa uzeeni basi unakuwa na kiasi cha kukusaidia kuendesha maisha yako.

7.  Anza kufanya kazi na anzisha kazi zako Binafsi.
Naam! Kazi ndio msingi mkubwa katika kuendesha maisha yetu ya kila siku. Iwe kazi ya kuajiriwa au kujiajiri, basi hakikisha unakuwa na kazi kabla ya kupita kwa umri huo.

Kazi yoyote ya halali ikifanywa vizuri, na kwa Ari basi inaweza kuleta tija kubwa katika maisha ya mtu.

Jitahidi kupata kazi ya halali itakayokuingizia kipato cha halali kabla ya kupitwa na ujana wako kwani wapo wazee wengi wanahadhirika maishani mwao kwa kushindwa kupata cha kujishughulisha nacho ujanani mwao.

8.  Kuwa na utaratibu wa kujisomea.
Alisema msomi mmoja kuwa, ukitaka kumfichia kitu mu Afrika, basi muwekee kwenye ktabu. Hii ina maana kuwa wa Afrika wengi, watanzania tukiwemo, hatuna utaratibu wa kujisomea.

Kwenye kujisomea kuna faida nyingi. Mbali na kufanya akili kuwa safi muda wote pia mtu anapata wasaa wa kujifunza vitu vipya ambavyo vinaweza kumsaidia maishani mwake kwa sasa na baadae pia.

Ni vizuri ukajiwekea utaratibu wa kujisomea vitabu, makala, magazeti n.k kuhusiana na masuala ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara na mambo mengine yanayohusu maisha.

9.  Jiunge na vikundi vya kijamii.
Kuna msaada mkubwa sana mtu kuwa kwenye vikundi vinavyofanya kazi za kuhudumia jamii. Vipo vikundi vya kifedha, michezo na utamaduni, afya, dini na vingine vingi. Ndani ya vikundi hivi unaweza kukutana na watu wapya mnaoweza kusaidiana katika maisha pia unaweza kutumia kama njia moja wapo ya kusaidia jamii inayokuzunguka.

10.    Acha! Acha! Acha! – Kuvuta Sigara, Ulevi, Uzinifu.
Asilimia kubwa ya vijana hupenda kuvuta sigara, ulevi na hata uzinifu. Kwa sasa huenda usiyaone madhara yake kwani ni vitu ambavyo huwa vinakula taratibu taratibu. Ila kwa miaka ya mbeleni unaweza kuja kukutana na madhara makubwa ambayo yanaweza kukufanya upoteze furaha ya maisha yako.

Jitahidi sana katika ujana wako kuojihusisha na uvutaji wa sigara, ulevi na uzinifu pia kwani gharama zake mbeleni ni kubwa mno.

11.    Funga ndoa.
Naam! Jitahidi sana kufunga ndoa kabla ya kupitwa na ujana wako. Mbali na kupata utulivu wa nafsi, ila itasaidia kuongeza uwajibikaji na umakini kwenye mambo mbalimbali ya maisha yako. Pia itasaidia kupata watoto mapema ambao wanaweza kuja kukusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yako ya mbeleni hasa katika shughuli zako za kila siku na Biashara zako kwa ujumla.

Kubwa ni kuheshimika katika jamii kwani asilimia kubwa ya watu waliopo kwenye ndoa huwa wanapewa heshima kubwa kwenye jamii zao na kushirikishwa kwenye baadhi ya majambo ya msingi.

12.    Kuwa na Ratiba.
Ni kawaida sana katika zama zetu kumkuta kijana hana jambo la kufanya. Yaani ukimkurupua kumwambia akusindikize sehemu, basi atakwenda muda huo huo na ukimuuliza huna la kufanya atakujibu ndio.

Ni vizuri kijana akapanga muda wake na kupanga mambo yake ya siku nzima. Jifunze kuweka ratiba ya kufanya mambo yako ya siku, wiki, mwezi na hata mwaka pia. Hii itakusaidia kufikia malengo yako ki urahisi na kutopata muda wa kufanya vitu visivyo na msaada maishani mwako.

13.    Tengeneza Mtandao wa watu watakaokusaidia. baadae
Kwa lugha ya kiingereza wanasema “Networking.” Jitahidi kuwa na network nzuri, yenye watu wazuri na wenye manufaa maishani mwako. Hakikisha kila mtu mzuri unayekutana nae unatengeneza nae mahusiano mazuri yatakayokunufaisha wewe na kumnufaisha yeye pia.

Hakikisha unapata marafiki kwenye kila idara ya kiuchumi, siasa, utamaduni na masuala ya kijamii pia.

14.    Mazoezi! Mazoezi! Mazoezi.
Hili ni jambo la msingi sana kwa kijana. Hakikisha unakuwa ni mwenye kufanya mazoezi walau mara mbili kwa wiki. Chagua mazoezi yatakayoendana na muda wako wa kazi na muda wako wa mambo mengine. Ni vizuri kufanya mazoezi asubuhi au/na jioni. Hii itasaidia kuuweka mwili wako vizuri na wenye afya muda wote. Vilevile itasaidia kukuweka mbali na magonjwa madogo madogo yanayoweza kupunguza ufanisi kwenye shuguli zako.

15.    Jifunze Lugha za Kigeni.
Dunia ya leo ni dunia ya utandawazi. Watu kutoka mataifa mbalimbali wanawekeza kwenye nchi za wengine. Ni vizuri ukajifunza lugha za kigeni hasa za mataifa yanayokuja kuwekeza kwenye nchi yako. Lugha itatanua wigo wako wa ajira, biashara, na hata kujua tamaduni za watu wengine.

16.    Jiweke mbali na madeni.

Hakuna kitu kinachorudisha nyuma watu kama vile madeni. Madeni humfanya mtu kila kipato anachopata kina kwenda kulipa madeni na badala ya kufanya maendeleo ya maisha yake. Hivyo jitahidi sana kuepuka madeni ndani ya umri huu. Kama kuna watu au taasisi inakudai basi fanya juu chini kulipa madeni hayo haraka na epuka kwa hali na mali kukopa (hasa mikopo yenye riba).
Soma Zaidi »

Thursday 30 June 2016

IJUE ZAKAATUL - FITRI


·        Maana Ya Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni zaka au sadaka ya lazima inayotolewa baada ya kumalizika Ramadhani, na kuingia tarehe mosi ya mwezi Shawwali (Mfungo Mosi). Imeitwa Zakatul – Fitri kwa sababu ni Zaka inayotolewa baada ya kufuturu (kumaliza Wajibu wa kufunga Ramadhani).

Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbas (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe Juu Yake) “Zaka ya Fiti ni kitakaso cha aliyefunga kutokana na mambo ya upuuzi na maneno machafu, na ni Lishe kwa masikini. Hivyo, atayeitoa kabla ya Swala, basi itapokewa kama Zaka, na ataye itoa baada ya Swala basi ni sadaka kama sadaka yoyote ile nyengine.”

Wanachuoni wa Fiqh, huielezea na Zaka ya Fitri kwamba: “ Zaka ya Fitri ni Sadaka ya uwajibu maalumu, ya kiwango maalumu, kutoka kwa mtu maalumu , kwa masharti maalumu, kwa niaba ya watu maalumu, kupewa watu maalumu; kwa lengo maalumu; nalo ni Kikataso cha Swaumu na Chakula kwa masikini.”

Zaka ya Firi imefaradhishwa mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili Hijriyya, kama kitakaso cha mwenye kufunga Ramadhani.


·        Wanaolazimikiwa Na Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni wajibu kwa kila nafsi Mwislamu aliyehai. Ni Zaka ya kiwiliwili, si zaka ya mali. Hivyo, midhali kiwiliwili kipo basi lazima kitolewe zaka ya Fitri. Ni wajibu. Ni Faradhi. Haiepukiki, isipokuwa kwa yule ambaye hana uwezo kabisa.

Ama mwenye kipato, au mwenye wajibu wa kumtunza mtu mwengine, kama mke, watoto, Wazee wake wawili wasiojiweza, watumishi wa nyumbani na kadhalika, na kipato chake kikawa kinazidi wajibu wake wa kuwatunza anaowatunza, basi ni wajibu kwake kujitolea yeye mwenyewe, kwanza, na kisha kuwatolea wote wale anaowajibika kuwatunza, kwa hali na mali. Yaani, lazima awe na chakula cha ziada ya kula yeye na familia yake, siku ya Idi.

Hicho kitachozidi ndicho kinachotolewa Zaka ya fitri. Kikiwa hakitosho kulisha family yake hiyo, siku ya Idi, basi hana jukumu la kutoa Zaka ya Fitri.

Kwa maneno mengine, iwapo baba mwenye nyumba ni masikini, hana cha kumtosha yeye na familia yake siku ya Idi, basi huyo hana wajibu wa kutoa zaka ya Fitri. Wala hana wajibu wa kumtolea mkewe, hata kama mke huyo ni mwenye uwezo kutokana na kipato chake mwenyewe.

Lakini mke, mwenye kipato chake mwenyewe, anaweza kujitolea kumtolea mumewe na watoto wake akipenda. Maana hana wajibu wa kujitunza, wala kumtunza mumewe wala watoto wake. Ni hiari yake, na ni fadhila kubwa, sana, kufanya hivyo. Ila SI wajibu juu yake.


·        Vinavyopaswa Kutolewa Kwenye Zakatul – Fitri na Viwango Vyake.
Kinachotakiwa Kutolewa kwenye Zakatul - Fitri ni chakula, na wala sio pesa. Na kiwango cha kutolewa ni pishi moja ya chakula kinacholiwa sana katika jamii husika. Hivyo, vyakula vinavyo ingia hapa ni nafaka zote, kuanzia ngano, shayiri, mchele, unga wa ngano, sembe, maharage, ulezi, na kadhalika. Ni chakula kinacholiwa sana na watu wengi katika jamii ya mtoa Zaka hiyo.

Kiwango cha Zaka ya Fiti ni Pishi moja, ambayo ni sawa na kilo mbili na grm 400; kwa pishi ya Mtume ï·º (Pishi ya Mtume ï·º ni sawa na vibaba vine, vya Mtume ï·º . Na kibaba kimoja ni ujazo wa nafaka kwenye viganja viwili kwa pamoja vya mtu wa kawaida.) Hivyo, ni kama kilo mbili na nusu za chakula kinachopendwa sana na jamii husika. Kiwango hicho ni kwa kila kiumbe, chenye uwezo wa kujitolea chenyewe.


·        Yakuzingatia Katika Utoaji wa Zakatul - Fitri
1.     Kuitoa mara baada ya kuandama mwezi wa Shawwal: yaani usiku wa kuamkia Siku Kuu, au kabla ya kwenda kuswali Swala ya Idi. Au kabla ya siku moja au mbili ya kumalizika Ramadhani.

2.     Kumtolea hata mtoto aliyetumboni, kama alivyokuwa akifanya Sayyidina Uthman bin ‘Affan رضي الله عنه . Ameipokea Ahmad na Ibn Abi Shayba.

3.     Kuigawa kwa mikono yako, mwenyewe, badala ya kuwapa watu wengine waitoe kwa niaba yako. Mtume ï·º akifanya hivyo, na kuwausia Maswahaba nao wafanye hivyo.

4.     Ukiwapa watoto wako nyumbani kuitoa, ni sawa na kuigawa mwenyewe.

5.     Kuwapa masikini jamaa zako, wenye kustahiki na ambao huna wajibu wa kuwatunza.

6.     Kuigawa kwa masikini wa mahali ulipo, ila ikiwa kuna wanaohitaji zaidi, na ni jamaa zako, nchi nyengine.

7.     Iwapo chakula unachotoa kina viwango mbali mbali, basi chagua kiwango cha juu: Mwenyezi Mungu amesema: “Hamtaipata Pepo mpaka mtoe mnavyo vipenda.”

8.     Kutoa nafaka kavu, inayoweza kuhifadhika kwa siku kadhaa bila ya kuharibika, ni bora kuliko chakula kisichoweza kuhifadhika kwa muda mrefu.

9.     Kwa upande wa Wazazi wako wawili, basi sunna kumtolea Mama mzazi kwanza, kisha ndiyo Baba mzazi – iwapo wanakutegemea kuwatunza.

10.           Kuwapa majirani zako masikini, ni bora kuliko masikini wa mbali.



Imechukuliwa kutoka katika Post ya Shaykh Shareef Abdulqader
Soma Zaidi »

Wednesday 29 June 2016

GESI YAGUNDULIKA TANZANIA


GESI ya helium ya takribani futi za ujazo bilioni 54 inayoelezwa kuwa adimu duniani, imegundulika nchini Tanzania na kuiweka nchi kuwa miongoni mwa mataifa machache yenye madini mengi na muhimu.

Wagunduzi wa gesi hiyo ni watafiti kutoka vyuo vikuu viwili nchini Uingereza vya Oxford na Durham kwa kushirikiana na wataalamu wa madini kutoka nchini Norway.

Watafiti hao wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi hiyo ya barafu, kama inavyofahamika katika eneo la Bonde la Ufa nchini.

Taarifa za waandishi wa habari nchini Japan, zimeeleza kuwa watafiti hao wamesema kuwa uhaba wa gesi hiyo duniani ulikuwa umesababisha taharuki haswa kwa madaktari, ambao wanatumia gesi hiyo adimu kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama ‘MRI scanners’.

Pia hutumia katika mitambo ya kinyuklia na katika sekta nyingine nyingi za kiteknolojia.

Wiki iliyopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akijibu swali bungeni mjini Dodoma alisema madini yanayotumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia vifaa vya matibabu kama MRI na NMR, yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi kiasi cha madini hayo na namna nchi itakavyonufaika na ugunduzi huo. Hata alipotafutwa jana, simu yake ya mkononi ilipokewa na msaidizi wake na kueleza kuwa waziri yuko kikaoni. Madini aina ya helium yanatumika kwa ajili ya mitambo na pia kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na NMR.

Kabla ugunduzi huo, watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo ifikapo mwaka wa 2035.
Mnamo mwaka 2010, mwanasayansi ambaye alikuwa mshindi ya Tuzo la Nobel, Robert Richardson alitabiri kumalizika kwa gesi hiyo katika kipindi kifupi. Ukosefu huo ulikuwa umesababisha wataalamu, kuhimiza kutungwa kwa sheria itakayopunguza matumizi yake katika bidhaa zisizo za dharura.

Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Chris Ballentine alisema gesi hiyo iliyopatikana nchini inaweza kujaza silinda za gesi milioni 1.2 za mashine za MRI.

Soma Zaidi »

Monday 16 May 2016

MKUTANO MKUBWA WA KIMATAIFA KUHUSU MIFUMO YA KIFEDHA YA KIISLAMU



Al-Huda Center of Islamic Banking & Economics (CIBE) ni taasisi inayojihusisha na utoaji elimu na mafunzo juu ya masuala ya Kibenki na Kifedha kwa utaratibu wa kiislamu duniani kote.

Kuelekea katika harakati za kutimiza malengo yake, taasisi hii imeandaa mkutano mkubwa unaokwenda kwa jina la "3rd African Islamic Finance Summit " utakaofanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa, May 19 & 20, 2016 katika hoteli ya Hyatt Regency Hotel Dar Es Salaam.

Dhumuni kubwa a mkutano huu ni kuelezea fursa mbalimbali zinazopatikana barani Africa na kujadili changamoto zinazokwamisha ukuaji wa masuala ya kibenki na mifumo ya kifedha ya kiislamu barani Africa.

Kwa maelezo zaidi kuhusu usajili na taarifa za undani juu ya mkutano huu bonyeza hapa.


Soma Zaidi »

KIWANDA CHA SUKARI MANYARA CHATAKA MIWA ZAIDI



KIWANDA cha Sukari cha Manyara (Manyara Sugar) kilichopo katika kijiji cha Matufa wilayani Babati mkoani Manyara, kimeiomba Halmashauri ya Wilaya ya Babati kusaidia kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima kulima miwa kwa wingi kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Meneja wa kiwanda hicho, Pratap Disodya aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kiwanda hicho hakina sababu ya kuficha sukari kwa kuwa kina uwezo wa kuzalisha tani 300 hadi 500 kwa siku.
Alisema pamoja na uzalishaji huo unaochangiwa na upungufu wa miwa kutoka kwa wakulima, kiwanda hicho pia kinalazimika kufungwa kila mwaka ifikapo Desemba hadi Juni kusubiri uzalishaji uanze Juni.
Alisema katika kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kuwataka wafanyabiashara wote walioficha sukari katika maghala yao kuanza kusambaza mara moja vinginevyo serikali itachukua hatua kali, kiwanda hicho kimethibitisha kutokuwa na akiba ya kutosha ya sukari inayozalishwa kiwandani hapo.
Alisema wakulima wakihimizwa kuzalisha miwa kwa wingi uzalishaji utaongezeka na kupunguza uhaba wa sukari nchini. Disodya alisema tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho mwaka 2005 na kuanza uzalishaji mwaka 2007, kimezalisha tani 150 mwaka 2013 pekee.
Alisema hatua walizochukua ni pamoja na uongozi wa kiwanda kuendelea kuwahamasisha wakulima wadogo zaidi ya 1,500 kuongeza uzalishaji wa miwa kwa kuwapatia mikopo.

Chanzo : Tovuti ya Habari Leo


Soma Zaidi »

Saturday 14 May 2016

HATUA 11 KUELEKEA UJASIRIAMALI WENYE MAFANIKIO


Imeandikwa katika Historia kuwa, wafanyabiashara wakubwa katika zama zilizopita hasa kwenye ukanda wa Mashariki ya kati ya dunia (Middle East) walikuwa ni Waislamu. Wao walizifanya shughuli zao za kiujasriamali kama Ibada na ni moja ya njia za kueneza dini na kutengeneza jamii yenye tabia njema iliyojaa uaminifu na uadilifu pia. Waliweza kufikia kilele cha juu kabisa cha maadili katika shughuli zao. Kwa ufupi tunaweza kusema, walikuwa ni wajasiriamali waliofanikiwa (Duniani na Akehra) jambo ambalo wajasiriamali wa karne hii ya 21 wamelipoteza

Zifuatazo ni hatua 11 za kuelea Ujasiriamlai wenye Mafanikio.

1.      Kuwa na Ikhalas.

Imesemwa katika Hadithi kuwa Matendo hulipwa kutokana na nia na kila mtu atalipwa matendo yake kulingana na nia aliyoiweka kwenye matendo hayo. Ifanye Biashara yako kama ni moja ya sehemu ya kupata Radhi za Mwenyezi Mungu. Kuwa na Ikhlas ndani yake na uifanye kwa kutegemea kuwa Allah atakulipa malipo yaliyo ya kheri kutokana na biashara hiyo.

2.      Fanya Istikhara.
Istikhara ni kumuomba Mwenyezi Mungu ushauri na ukupe maamuzi yaliyo na kheri nawe kwenye jambo linalokutatiza. Allah ndiye nayetujua zaidi kuliko tunavyojiujua sisi wenyewe. Ni vizuri kufanya Istikhara kabla ya kuanza biashara zetu na kumuomba Allah akupe yaliyo na kheri kwenye biashara yako hiyo. Jifunze Jinsi ya Kuswali swala ya istikhara hapa.

3.      Fanya Shura.

Mwenyezi Mungu amewasifu waumini kwa sifa ya kufanya majambo yao na kuyapeleka kwa mfumo wa “Shura” (42:38). Shura ni kutafuta ushauri na maoni juu ya jambo Fulani kutoka kwa watu wengine. Ni vizuri ukapata ushauri juu ya Biashara yako kutoka kwa wataalamu waliobobea na wenye kuaminika kulingana na bishara uliyonayo.

4.      Jielimishe.
Moja kati ya Sifa za Mjasiriamali wa Kiislamu ni kupenda kujielimisha. Kujielimisha huku kunatakiwa kuanzie mwanzoni na kuendelea nako kwenye mchakato mzima wa kuelekea bishara yenye mafanikio. Jielimishe kupitia Vitabu sahihi vinavyohusu Biashara yako, hudhuria semina na ikiwezekana jiunge na kozi mbalimbali zitakazokusaidia kuwa madhubuti kwenye Biashara yako.

5.      Angalia Mtaji Wako.

Moja kati ya maswali ya kujiuliza mjasiriamali akiwa kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ni mtaji wake. Ni lazima ajue anahitaji kiasi gani cha mtaji na wapi atapata mtaji huo. Ni vizuri kwa mjasiriamali wa kiislamu ahakikishe biashara yake inaanzishwa na mtaji wa halali na anaouridhia Mwenyezi Mungu. Pia ni lazima aanzishe biashara inayoendana na mtaji wake na achunge mtaji huo usije ukapotea kizembezembe.

6.      Angalia Fursa Zilizopo.

Usije kuanzisha Biashara ambayo sio Fursa kwani huenda ukakosa muendelezo mzuri wa biashara hiyo. Ni lazima uangalie Fursa zilizopo ndani ya biashara unayotaka kuanzisha na hata nje ya biashara yako hiyo. Angalia fur’sa za halali na zenye kuleta tija katika jamii inayokuzunguka.

7.      Weka Ratiba Madhubuti.

Si katika maisha ya kila siku tu, hata kwenye masuala ya ujasiriamali, suala la ratiba lina umuhimu mkubwa sana. Sio Ratiba tu ilimradi ratiba, ila ni ratiba madhubuti. Hakikisha unaandaa ratiba nzuri ya shughuli zako kwa kuzingatia masuala ya kiibada, kijamii, kiafya n.k

8.      Simamia Malengo Yako.

Mafanikio ya kwenye maisha yako ya duniani na akhera yapo kwenye mikono yako mwenyewe. Ukiwa kama mjasiriamali wa kiislamu ni lazima uhakikishe unasimamia malengo yako uliyojiwekea. Usikubali kuyumbishwa (bila sababu ya msingi). Kila siku kabla ya kulala ni lazima ujifanyie hesabu ni kwa kiasi gani umeyafikia malengo uliyoyakusudia, na kila unapoamka lazima ujiwekee njia utakazotumia kwa siku hiyo kuyafikia malengo hayo.

9.      Tengeneza Mtandao wenye Manufaa.

Hakuna jambo zuri kwenye maisha na kwenye ujasiriamali (hasa wa kiislamu) kama mtu kuwa na mtandao wenye manufaa. Hakikisha unazungukwa na watu ambao watakusaidia kwa namna moja ama nyingine kufikia malengo uliyoyakusudia. Hakikisha unakuwa na mawasiliano yao ya simu, barua pepe (email), na kujua sehemu zao za kazi na vipi wataweza kukusaidia kwenye kutimiza malengo yako.

10.  Jifunze Kutokana na Makosa.

Asilimia kubwa ya watu wasiojifunza kutokana na makosa (aidha waliyoyafanya wao au yaliyofanywa na wengine) huwa wana tabia ya kurudia makosa yaleyale. Kama mjasiriamali wa kiislamu ni lazima ujue ulipokosea na uweke mikakati madhubuti ya kutorudia tena makosa hayo.

11.  Safisha Mali Zako.

Naam usafi wa mali ni jambo la muhimu sana kwa mjasiriamali wa kiislamu. Jambo hili limesahaulika mno na wajasiriamali wengi wa kiislamu. Njia kuu ya kusafisha mali zako ni kwa Kutoka zaka (kama kiwango cha mali zako kinafikia kutoa zaka). Njia zingine ni kutoa sadaka, kusaidia wanafunzi malipo yao ya masomo, kusaidia masikini n.k

Kwa Muislamu, Ujasiriamali ni sehemu ya Ibada na ni moja ya njia zinazoweza kutumika kuufikisha uislamu katika ubora wake. Ni vizuri tukawa na malengo makubwa ya kufanya shughuli zetu za kiujasiriamali ni zenye kufanikiwa kwa kufuata kanuni na sheria zilizopo kwenye uislamu insha allah.

Maassalaam.
Soma Zaidi »