Thursday 30 June 2016

IJUE ZAKAATUL - FITRI


·        Maana Ya Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni zaka au sadaka ya lazima inayotolewa baada ya kumalizika Ramadhani, na kuingia tarehe mosi ya mwezi Shawwali (Mfungo Mosi). Imeitwa Zakatul – Fitri kwa sababu ni Zaka inayotolewa baada ya kufuturu (kumaliza Wajibu wa kufunga Ramadhani).

Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbas (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe Juu Yake) “Zaka ya Fiti ni kitakaso cha aliyefunga kutokana na mambo ya upuuzi na maneno machafu, na ni Lishe kwa masikini. Hivyo, atayeitoa kabla ya Swala, basi itapokewa kama Zaka, na ataye itoa baada ya Swala basi ni sadaka kama sadaka yoyote ile nyengine.”

Wanachuoni wa Fiqh, huielezea na Zaka ya Fitri kwamba: “ Zaka ya Fitri ni Sadaka ya uwajibu maalumu, ya kiwango maalumu, kutoka kwa mtu maalumu , kwa masharti maalumu, kwa niaba ya watu maalumu, kupewa watu maalumu; kwa lengo maalumu; nalo ni Kikataso cha Swaumu na Chakula kwa masikini.”

Zaka ya Firi imefaradhishwa mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili Hijriyya, kama kitakaso cha mwenye kufunga Ramadhani.


·        Wanaolazimikiwa Na Zakatul - Fitri
Zakatul - Fitri ni wajibu kwa kila nafsi Mwislamu aliyehai. Ni Zaka ya kiwiliwili, si zaka ya mali. Hivyo, midhali kiwiliwili kipo basi lazima kitolewe zaka ya Fitri. Ni wajibu. Ni Faradhi. Haiepukiki, isipokuwa kwa yule ambaye hana uwezo kabisa.

Ama mwenye kipato, au mwenye wajibu wa kumtunza mtu mwengine, kama mke, watoto, Wazee wake wawili wasiojiweza, watumishi wa nyumbani na kadhalika, na kipato chake kikawa kinazidi wajibu wake wa kuwatunza anaowatunza, basi ni wajibu kwake kujitolea yeye mwenyewe, kwanza, na kisha kuwatolea wote wale anaowajibika kuwatunza, kwa hali na mali. Yaani, lazima awe na chakula cha ziada ya kula yeye na familia yake, siku ya Idi.

Hicho kitachozidi ndicho kinachotolewa Zaka ya fitri. Kikiwa hakitosho kulisha family yake hiyo, siku ya Idi, basi hana jukumu la kutoa Zaka ya Fitri.

Kwa maneno mengine, iwapo baba mwenye nyumba ni masikini, hana cha kumtosha yeye na familia yake siku ya Idi, basi huyo hana wajibu wa kutoa zaka ya Fitri. Wala hana wajibu wa kumtolea mkewe, hata kama mke huyo ni mwenye uwezo kutokana na kipato chake mwenyewe.

Lakini mke, mwenye kipato chake mwenyewe, anaweza kujitolea kumtolea mumewe na watoto wake akipenda. Maana hana wajibu wa kujitunza, wala kumtunza mumewe wala watoto wake. Ni hiari yake, na ni fadhila kubwa, sana, kufanya hivyo. Ila SI wajibu juu yake.


·        Vinavyopaswa Kutolewa Kwenye Zakatul – Fitri na Viwango Vyake.
Kinachotakiwa Kutolewa kwenye Zakatul - Fitri ni chakula, na wala sio pesa. Na kiwango cha kutolewa ni pishi moja ya chakula kinacholiwa sana katika jamii husika. Hivyo, vyakula vinavyo ingia hapa ni nafaka zote, kuanzia ngano, shayiri, mchele, unga wa ngano, sembe, maharage, ulezi, na kadhalika. Ni chakula kinacholiwa sana na watu wengi katika jamii ya mtoa Zaka hiyo.

Kiwango cha Zaka ya Fiti ni Pishi moja, ambayo ni sawa na kilo mbili na grm 400; kwa pishi ya Mtume (Pishi ya Mtume ni sawa na vibaba vine, vya Mtume . Na kibaba kimoja ni ujazo wa nafaka kwenye viganja viwili kwa pamoja vya mtu wa kawaida.) Hivyo, ni kama kilo mbili na nusu za chakula kinachopendwa sana na jamii husika. Kiwango hicho ni kwa kila kiumbe, chenye uwezo wa kujitolea chenyewe.


·        Yakuzingatia Katika Utoaji wa Zakatul - Fitri
1.     Kuitoa mara baada ya kuandama mwezi wa Shawwal: yaani usiku wa kuamkia Siku Kuu, au kabla ya kwenda kuswali Swala ya Idi. Au kabla ya siku moja au mbili ya kumalizika Ramadhani.

2.     Kumtolea hata mtoto aliyetumboni, kama alivyokuwa akifanya Sayyidina Uthman bin ‘Affan رضي الله عنه . Ameipokea Ahmad na Ibn Abi Shayba.

3.     Kuigawa kwa mikono yako, mwenyewe, badala ya kuwapa watu wengine waitoe kwa niaba yako. Mtume akifanya hivyo, na kuwausia Maswahaba nao wafanye hivyo.

4.     Ukiwapa watoto wako nyumbani kuitoa, ni sawa na kuigawa mwenyewe.

5.     Kuwapa masikini jamaa zako, wenye kustahiki na ambao huna wajibu wa kuwatunza.

6.     Kuigawa kwa masikini wa mahali ulipo, ila ikiwa kuna wanaohitaji zaidi, na ni jamaa zako, nchi nyengine.

7.     Iwapo chakula unachotoa kina viwango mbali mbali, basi chagua kiwango cha juu: Mwenyezi Mungu amesema: “Hamtaipata Pepo mpaka mtoe mnavyo vipenda.”

8.     Kutoa nafaka kavu, inayoweza kuhifadhika kwa siku kadhaa bila ya kuharibika, ni bora kuliko chakula kisichoweza kuhifadhika kwa muda mrefu.

9.     Kwa upande wa Wazazi wako wawili, basi sunna kumtolea Mama mzazi kwanza, kisha ndiyo Baba mzazi – iwapo wanakutegemea kuwatunza.

10.           Kuwapa majirani zako masikini, ni bora kuliko masikini wa mbali.



Imechukuliwa kutoka katika Post ya Shaykh Shareef Abdulqader

No comments:

Post a Comment